You are currently viewing MKE WA MUME WANGU

MKE WA MUME WANGU

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 45 aliwashangaza watu baada ya kuhudhuria ndoa ya mume wake na kumkaribisha mke mwenza kwenye familia. Kulingana na mwanamke huyo, amemkubali mke mwenza ambaye ana umri wa miaka 26 na kusema kuwa yuko tayari kumpokea mke wa mumewe.

Harusi hiyo iliyofanyika katika kanisa la Africa Kusini, International Pentecost Holiness Church(IPHC) iliwavutia wengi kuhudhuhuria ambapo hadithi hii ilijitokeza na kuwa habari. Mwanamke huyo alisema kuwa kukubali kwake kumetokana na imani yake na kusema kuwa moyo wake ulikuwa na furaha kwani alimjua mwanadada huyo ambaye angekuwa mke mwenza.

Akieleza zaidi, alisema kuwa alipomuona dada yule alimpenda na kutaka mumewe kumuoa. Baada ya kuendelea kwa makubaliano, hatimaye mumewe alimuoa dada yule kanisani. Mwanamke huyo alisema kuwa haja ya moyo wake imekuwa ni kupanua familia yake na kupitia ndoa hii, ndoto yake imetimia.

Mwanamke huyo alisema kuwa kwa kushuhudia misa ya harusi ile, hatimaye amepata mke mwenza aliyekuwa akimsubiri kwa miaka. Mwanamke huyo alihudhuria misa ya harusi ya mumewe mwenye umri wa miaka 49 akimuoa binti wa miaka 26 na kuikubali ndoa ile.

Wawili hao wamejaliwa na watoto watatu na sasa wanatarajia kuipanua familia zaidi.Jambo hili lilizua gumzo mtandaoni ambapo watu walitoa hisia tofauti ambapo wengi walishangazwa na jinsi mwanamke huyo alivyokubali ndoa ile.

Kutokana na hoja za wanawake wengi walisema kuwa hawakubaliani na kupata mke mwenza huku wanaume wengi wakisema wanatamani kupatana na mwanamke kama yeye.Tukio hili liliwastaajabisha wengi kwani ni nadra sana kutokea.

Mwandishi, Jane Mwangi.