Kupitia mtandao rasmi wa twitter, ya Hifadhi ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki, kifo cha ndovu afahamikaye kama Dida kilichapishwa siku ya jumanne. Aidha, kifo chake kilidhibitishwa baada ya mifupa ya ndovu huyo kupatikana iliyoonyesha kuwa tembo huyu alifariki miezi kadhaa iliyopita. Dida alifahamika zaidi kama mama mlezi katika mbuga ya kitaifa ya Tsavo Mashariki. Aidha, pembe zake zilimfanya kuwa mashuhuri zaidi kutokana na urefu.
Tembo huyu wa jike alikuwa ndiye mkongwe zaidi kwani ameaga akiwa na umri wa miaka 65. Kikundi cha Uhifadhi cha Tsavo Trust kilimsifu Dida kama mfano halisi na wa kipekee atakayekumbukwa na vizazi vijavyo vya tembo. Aidha, KWS ilikanusha madai kuwa tembo huyu aliaga kutokana na makali ya njaa yalkiyosababishwa na ukame ulioko nchini na kusema Dida alifariki kutokana na asili zinazoletwa na ukongwe.
Kwa kumuomboleza Dida, KWS ilisema kuwa amekuwa hazina kubwa ya maarifa ya miongo mingi.Alihudumu kama somo la filamu mbalimbali na alikuwa kivutio cha watalii.
By Jane Mwangi.