Posa ya mwanaume mmoja katika kaunti ya Tana River yageuka kuwa taabu baada ya mpenzi wake aliyetaka kumchumbia kuimeza pete ile. Johanna Charo alipanga kumchumbia mpenzi wake Jessica Hawayu kwa njia ambayo kwake aliamini ni ya kimahaba na itakayompendeza mpenzi wake.
Kwa usaidizi wa familia ya Jessica, waliamua kuandaa pilau kwani ndicho chakula alichokipenda babake Jessica zaidi. Jessica alisaidia katika maandalizi ya chakula hicho akidhani anamwandalia babake. Baada ya kuandaa chakula hicho, waliiweka pete ndani ya pilau ya Jessica bila kumwarifu kwani walitaka iwe ‘surprise’ lakini mambo yalienda mrama baada ya Jessica kuimeza pete ile.
Kulingana na dadake Jessica, alisema kuwa babake alikuwa amekataa mpango huo kwani alikuwa na shauku lakini mwishowe waliamua kuendelea nao kwani hawakufikiria jinsi nyingine ambayo wangeitekeleza posa ile. Kulingana na kakake Jessica, hakuna aliyetarajia hili kutokea ispokuwa baba yake aliyekuwa hakubaliani na mpango huo.
Jessica alinusurika baada ya babake kumgonga mgongoni ili kuilazimisha pete ile kutoka. Kutokana na mshtuko wa kilichojiri, Jessica alipoteza fahamu na kupelekwa hospitalini ili kupata matibabu. Johanna Charo alisema kuwa amepata funzo kwani ameponea kumpoteza mpenzi wake.
Mwandishi, Jane Mwangi.